YASIKITISHA SANA MTOTO WA MIAKA 12 AMEPOTEZA MAISHA BAADA YA KUTAIRIWA KIENYEJI.
Asheri Selemani (12), amefariki dunia baada ya kutahiriwa kienyeji, huko wilayani Chamwino.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa kwa waandishi wa habari June 9 jijini Dodoma, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, tukio hilo limetokea katika kijiji cha Mlodaa kilichopo kata ya Mlowa barabarani.
Alifafanua kuwa mwanafunzi huyo alifariki dunia baada ya kuvuja damu nyingi kutokana na kutahiriwa kienyeji na ngariba.
Hata hivyo, alisema baada ya tukio hilo ngariba huyo alitoroka na kutokomea kusikojulikana na jitihada za kumtafuta bado zinaendelea.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoani humo linawashikilia watu 35 kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kihalifu katika maeneo mbalimbali mkoani hapa.
Alifafanua kuwa watu watatu wanashikiliwa kwa kuiba vifaa vya mafunzo ya Tehama (tablet) 48 aina ya huawei na projekta moja zilizoibiwa katika Shule ya Msingi St Gaspar ya Miyuji, jijini hapa.
Alitaja thamani ya vifaa hivyo kuwa ni Sh. milioni 56 na vifaa hivyo ni vya mradi maalumu wa mafunzo ya Tehama katika shule za msingi nchini na Mkoa wa Dodoma mradi huo upo katika shule 10.
Alisema vifaa hivyo vimekamatwa na jeshi hilo baada ya msako katika maeneo mbalimbali mkoani hapa na vingine kukamatwa mikoa ya Dar es Salaam na Arusha.
Aliwataja watuhumiwa wanaoshikiliwa kwa kudaiwa kuhusika na tukio hilo kuwa ni Nathanael Mkenda (25) mwanafunzi wa chuo cha madini,Timoth Mapunda (19) fundi seremala na Benedict Mkinga (17) mwanfunzi kidato cha pili Shule ya John Merlini.
Katika tukio la pili, watuhumiwa wawili Peter Kihanda (28) mkazi wa Kahama mkoani Shinyanga na Ramadhani Bakari Dereva wa lori namba T 105 CYL, mali ya kampuni ya Simera Tansport Ltd., wanashikiliwa kwa kusafirisha bangi vifurusi sita vyenye uzito wa kilo 162.
Hata hivyo, Kamanda Muroto alisema katika tukio lingine walimkamata Manka James, mkazi wa Isamilo mkoani Mwanza kwa kudaiwa kujihusisha na utapeli wa kuwarubuni watu na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu maeneo ya benki.
Aidha, alisema katika msako huo waliwakamata wahalifu wa kijihusisha na ukabaji na uporaji nyakati za usiku katika maeneo mbalimbali ya jiji na wengine wizi wa majumbani pamoja na pikipiki.
Muroto alisema watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Aliwashukuru wananchi kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao hivyo aliwaomba kuendelea kutoa taarifa za wahalifu katika maeneo yao na jeshi hilo watazifanyia kazi.
“Jeshi la Polisi tunafanya msako wa kuwatafuta wahalifu nyumba kwa nyumba hadi sikukuu ya Idd itakapofika,tunataka wahalifu wakasherehekee sikukuu hiyo wakiangalia kuta za magereza kwa sababu hawataki kuwa raia wema”alisema Muroto.